Jumapili , 17th Feb , 2019

Baada ya kusambaa mitandaoni kwa sauti inayodaiwa kuwa ni ya Naibu Waziri, Mwita Waitara kuhusu kutovumiliwa kwa msaliti, Mbunge wa Kawe Halima Mdee amesema kwamba kauli hiyo inaonyesha serikali imekiri kuhusika na shambulio la Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Antiphas Lissu.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee

Mdee amechapicha ujumbe huo kwenye ukurasa wae Twitter baada ya kuenea kwa sauti hiyo ambayo imekosoa vikali ziara za nchi za ulaya na Marekani zinazofanywa na Mbunge Tundu Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi Septemba 07, 2017 nje ya nyumbani kwake Jijini Dodoma.

Sauti hiyo inasema kwamba, "mnapokuwa kwenye mapambano, hasa vita vya uchumi, ili nchi itoke ianze kujitegemea, tupange mambo yetu wenyewe sasa yeye anataka turudi tulipokuwa. Kwenye vita kama mkiwa mstari wa mbele halafu mwenzenu anawakwamisha mnamuwaisha yeye. Huu ni utaratibu wa mapambano".

Imeendelea kusema, "kama ukiwa mzalendo ukipotea gharama itatumika kukutafuta lakini kamwe siyo kumtafuta msaliti".

Baada ya kauli hiyo Mdee amesema kwamba, "damu ya mtu haijawahi kumuacha mtu salama...Naona serikali inakiri kuhusika na shambulio la kutaka kumuua tundu lissu..na kwamba mipango ya kutaka kumuua bado inaendelea".

Mbali na Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche ameeleza kwamba Watanzania hawatakubaliana na matukio yanayopangwa kudhuru viongozi wa vyama vya upinzani.

"Hizi kauli za kiitarahamwe na za kipuuzi zinazotolewa kuhusu kudhuru viongozi wa upinzani haziwezi kupuuzwa. Kwa yeyote anaepanga majaribio haya ajue wanachama na Watanzania hawatakubali upumbavu huu. Upinzani upo kwa sheria haiwezekani watu wanatishia wenzao kuwaondoa duniani".

Hata hivyo harakati za kumtafuta Naibu Waziri, Waitara kufafanua kauli zake ziligonga mwamba baada ya simu yake ya mkoni kutopatikana.

Sikiliza sauti hiyo hapa chini