Alhamisi , 19th Apr , 2018

Serikali kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, imesema zoezi la kuhamasisha kina mama waliotelekezwa na wazazi wenzao kwenye malezi ya watoto lililoendeshwa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Mkonda lipo sahihi na hajakosea.

Akijibu hoja za wabunge mbali mbali Bungeni, Waziri Ummy Mwalimu amesema zoezi hilo lilikuwa halali kwa sababu lipo chini ya kifungu cha sheria ya watoto ya mwaka 2009, ingawa kweli kulikuwa na makosa ambayo waliyafanyia kazi.

Waziri Mwalimu amesema sheria hiyo inawaruhusu maafisa wa ustawi wa jamii kusimamia suala la malezi ya mtoto pale familia inapofarakana, na Paul Makonda alipitia mgongo wa ustawi wa jamii ambayo pia ipo chini ya ofisi yake.

Zoezi lilikuwa ni halali, kwa sababu sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009, inatoa mamlaka kwa kamishna wa ustawi wa jamii kusimamia matunzo na malezi, zoezi lile liliendeshwa na maafisa wa ustawi wa jamii, suala lililojitokeza ni suala la faragha na kulinda haki za mtoto, baada ya kutoa tahadhari ile, sasa hivi zoezi linaendeshwa bila ku-expose sura za watoto, alichofanya makonda ni kuwahamasisha wanawake waende”, amesema Ummy Mwalimu.

Sambamba na hilo Waziri Ummy Mwalimu amesema wananchi wana changamoto kubwa ya kutokuwa na uelewa wa kupeleka mashtaka ya malezi ya watoto kwa ustawi wa jamii, na kuishia kubaki na mzigo wa kulea familia peke yao.

Zoezi hilo ambalo limeendeshwa na RC Makonda, limetuhumiwa kukiuka haki za mtoto, huku baadhi ya viongozi na wabunge wakilaumu na kusema kwamba suala la malezi ya mtoto ni suala la faragha na sio la kuliweka wazi kwenye jamii, huku wakitaka kiongozi huyo kuwajibishwa kwa kukiuka masuala hayo.