
Eneo la 14 Riverside, Nairobi nchini Kenya.
Update:
Mkuu wa Jeshi la Polisi Kenya IGP Joseph Boinnet, amesema ghorofa sita kati ya saba za hoteli ya Dusit zimekaguliwa na polisi ambapo watu watano wamefariki ndani ya hoteli hiyo iliyovamiwa na watu wenye silaha huku kundi la kigaidi la Al-Shabab likidai kuhusika.
Update:
Mkuu wa Jeshi la Polisi Kenya IGP Joseph Boinnet amethibitisha kutokea kwa shambulizi hilo leo saa 9:00 mchana, ambapo amesema kuwa hali kwa kiasi fulani imedhibitiwa kwa sasa na polisi wanaendelea kuwasaka wahusika.
IGP Boinnet amesema kuwa wanafahamu kuwa bado kuna baadhi ya wahalifu ndani ya jengo hilo na polisi watapambana nao na kuwadhibiti katika muda usio mrefu na kurejesha hali ya amani katika eneo hilo la hoteli ya DusitD2.
Awali wakati zoezi hilo likiendelea polisi walibaini bomu na kulitegua bila kuleta madhara yoyote lililokuwa kwenye gari moja dogo aina ya Totota IST, ambapo pia wamelipekuwa na kutoa sanduku lililokuwa na nyaraka kadhaa.
Hospitali ya Avenue Jijini Nairobi imepokea majeruhi 9 wa shambulizi la Hoteli ya Dusit ambapo mmoja wao akiwa ni mama mjamzito. Pia hospitali ya Kenyatta nayo imepokea majeruhi watano ambao wana majeraha ya risasi.
Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya, limeomba watu kujitokeza kutoa msaada wa damu kwa ajili ya majeruhi katika hospitali ya Avenue.
Kenya inakumbukumbu ya shambulizi la kigaidi la Septemba 21 mwaka 2013 Jijini Nairobi liliuwa watu 67 na kujeruhi wengine kadhaa, ambapo watuhumiwa watatu wa tukio hilo kesi yao itasikilizwa Januari 21, mwaka huu.
Mkuu wa polisi wa uchunguzi wa jinai Bw. George Kinoti ni miongoni mwa maafisa wakuu wa polisi waliofika kuratibu operesheni ya kuokoa watu waliokwama ndani ambapo amekiri kuwa bado uchunguzi unaendelea na hawajabaini wahalifu.
Eneo hilo lenye hoteli ya kifahari na ofisi za kampuni mbalimbali, baadhi ya watu waliokwama kwenye vyumba vya jumba hilo wamekuwa wakiandika ujumbe kwenye mitandao wa kijamii wakieleza kwamba wamekwama na kueleza mahali walipojificha ili kupata msaada.
Milipuko miwili mikubwa ilisikika na baadaye ufyatuaji wa risasi, ambapo tayari baadhi ya majeruhi amesafirishwa kupelekwa hospitali.