Sherehe zapigwa marufuku

Saturday , 12th Aug , 2017

Mkuu wa wilaya ya Kilombero James Ihunyo amepiga marufuku mtu yeyote kufanya sherehe bila kibali kutoka kwa mtendaji wa eneo husika ikiwa ni pamoja na kuuza chakula kiholela kama njia ya kuthibiti utumiaji hovyo wa chakula.

Ihunyo amesema ameamua kupiga marufuku hiyo ili kuthibiti utumiaji hovyo wa chakula kilichopatikana msimu huu wa mavuno na kujikinga na baa la njaa katika wilaya yake. 

Mkuu wa wilaya hiyo ya Kilombero akiongea leo kwenye kikao cha baraza la madiwani la mji wa Ifakara Ihunyo amesema serikali yake ya wilaya imejipanga kuhakikisha sherehe zisizo za lazima hazifanyiki na kuwataka Watendaji na Madiwani kushirikiana kukemea vitendo hivyo.

Mbali na hilo Diwani wa Kata ya Viwanja Stini amelalamika ucheleweshaji wa fedha kutoka serikali kuu na kudai jambo hilo linakuwa linakwamisha mipango ya maendeleo katika halmshauri hiyo na kata zake.  

Awali kabla ya kikao hicho kuanza Mbunge viti maalum mkoa wa Morogoro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mchungaji Getruda Lwakatare aliapishwa kuwa mjumbe kamili wa baraza hilo la madiwani.