Jumatatu , 11th Nov , 2019

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, amesema kuwa hadi kufikia Ijumaa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litaipitisha Sheria inayotoa mamlaka kwa mtu kujipima UKIMWI.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu

Hayo ameyabainisha leo Novemba 11, 2019 wakati wa ufunguzi wa semina elekezi kwa wasanii mbalimbali iliyoandaliwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa pamoja na Baraza la watu wanaoishi na UKIMWI (NACP).

“Changamoto kubwa inayoikabili Wizara ya Afya katika suala zima la VVU na UKIMWI ni wanaume kutojitokeza kwa wingi kupima, na hapa ninavyoongea leo hadi Ijumaa sheria ya watu kujipima wenyewe Virusi vya UKIMWI majumbani kwao itapitishwa rasmi, lakini hata hivyo itampasa mtu kwenda hospitali kupima tena ili ajiridhishe hata kama atakuwa ameshajipima mwenyewe” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy ameongeza kuwa Wizara yake imepeleka mapendekezo ya sheria itakayoruhusu umri wa mtu kupima Virusi vya Ukimwi uanzie miaka 15.

Aidha Waziri Ummy ametoa rai kwa wasanii wote waliohudhuria semina hiyo kutumia wafuasi wao walionao kupitia matamasha na hata mitandao ya kijamii kutoa elimu sahihi juu ya VVU na UKIMWI mwenyewe ili kutimiza lengo la Serikali la kuwa na asilimia 0 ya maambukizi mapya ifikapo mwaka 2030.