"Shida siyo Lowassa kwenda Ikulu" - BAVICHA

Alhamisi , 11th Jan , 2018

Katibu Mkuu wa (BAVICHA) Julius Mwita amefunguka na kusema kitendo cha Mhe. Edward Lowassa kwenda kukutana na Rais Ikulu siyo tatizo ila tatizo ni kumsifia kiongozi huyo wakati ambao kuna mambo mengi hayaendi sawa. 

Mwita amesema hayo leo wakati akiongea na waandishi wa habari na kudai kuwa msimamo wa BAVICHA ni ule ambao umetolewa na Mwenyekiti wa chama chao kuwa kauli alizotoa Edward Lowassa kwa Rais ni maoni yake binafsi na si msimamo wa chama chao. 

"Leo hatuwezi kumsifu Rais, tunampongeza kwa jambo gani kwamba Tundu Lissu ameshambuliwa na washambuliaji hawajakamatwa mpaka sasa au tunampongeza kwa sababu uchumi wa nchii hii ume 'collapse' sisi BAVICHA tunaunga kauli ya Mwenyekiti kwamba alichosema Lowassa ni kauli yake yeye na mtizamo wake yeye na sisi wanachama wetu wana uhuru ndiyo maana chama chetu kimeitwa Chama Cha Demokrasi na Maendeleo kwamba una uwezo wa kukutana na mtu yoyote mahali popote na ukazungumza kile ambacho ni mtazamo wako na si mtazamo wa chama" alisema Mwita 

Aidha Mwita amesema kuwa yeye hawezi kusema kwamba Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa amewasaliti CHADEMA kwa kauli zake hizo kwa kuwa hajapingana na msimamo wa chama bali ametoa mawazo yake binafsi.

"Sisi BAVICHA hatujamlaumu Lowassa kwa yeye kumsifu Magufuli ila tumehoji katika mazingira ya sasa, mazingira ambayo Spika wa Bunge anaamua kumfukuza Mbunge wa CHADEMA kukaa nje mwaka mzima wewe mwanachama wa CHADEMA na Mjumbe wa Kamati Kuu unatoa wapi ujasiri wa kumpongeza Magufuli. Katika wakati ambao msaidizi wa Mwenyekiti wa chama hajulikani sasa mwaka na kitu, katika wakati ambao taifa halijui mustakabali wake wa uchumi kesho unatoa wapi ujasiri wa kumsifia Rais" aliuliza Mwita 

Mbali na hilo Julius Mwita alisema kuwa kama kiongozi huyo atafikiri kurudi kwenye chama chake cha awali CCM waoa wala hawana tatizo na kuhofia kwani wapo viongozi wengi wametoka ndani ya chama hicho na chama kimezidi kuwa imara zaidi. 

"Lowassa akiamua kurudi CCM sisi hatuwezi kuogopa bali tutamshukuru kwa kipindi chote amekaa na sisi na tutamtakia maisha mema kama ambavyo tumewatakia maisha mema viongozi wote waliondoka CHADEMA kwenda CCM kwa sababu Katiba ya nchi hii inampa uhuru mwananchi yoyote ama kuwa na chama au kutokuwa na chama, ukiamua kuwa na chama bado utaamua wewe uwe katika chama gani CHADEMA, TLP au chama kingine chochote siku ukiamua kutoka NCCR kwenda chama kingine hawawezi kukuzuia kutoka' alisema Mwita