Alhamisi , 18th Oct , 2018

Ikiwa imetimia siku ya saba tangu kupotea kwa mfanyabiashara na bilionea kijana maarufu Afrika Mohamed Dewji wanasiasa mbalimbali bila kujali itikadi za vyama vya siasa wameoneshwa kuguswa kwa hisia tofauti juu ya tukio hilo.

Mfanyabiashara Mohamed Dewji

Www.eatv.tv imefuatilia baadhi ya wanasiasa wenye nguvu kubwa ya ushawishi kwenye mitandao ya  kijamii nchini wanaotokea Chama cha Mapinduzi CCM, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Act- Wazalendo pamoja na Chama Cha Wananchi (CUF).

Kwa upande wa CCM, miongoni mwa watu ambao walionesha kuguswa na tukio la kupotea kwa Mohamed Dewji ni Waziri wa zamani wa Mambo ya ndani ya nchi, Dkt Mwigulu Nchemba, ambaye siku ya tukio la kutekwa kwa Mo Dewji aliandika “Comrade,this too shall pass..Nakuombea uwe salama”, akimaanisha kuwa hili nalo litapita na kumuombea kwa Mungu mfabiashara huyo apatikane.

Kada mwingine wa CCM aliyeonesha kuguswa na tukio hilo ni Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ambaye nae alichapisha picha ya Mo Dewji na kuandika ujumbe “ooh GOD na kuweka alama (emoji) ikionesha akibubujikwa na machozi.

Mbunge wa Nzega mjini, Hussein Bashe ambaye nae aliandika “inasikitisha na kustua tukio hili la @moodewji kutekwa aina hii ya uhalifu inaota mizizi, ana familia ana watoto ana ndugu,  tuendelee kumuombea kwa Allah na kila mmoja wetu kutoa taarifa yoyote atakayopata ambayo itasaidia kumpata akiwa salama Allah amlinde."

Mbali na wabunge hao CCM, Mbunge mwingine wa CHADEMA ambaye ni Waziri kivuli wa mambo ya  ndani ya nchi, Godbless Lema ambaye nae wakati tukio hilo likitokea, aliandika “kama Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani,ninafuatilia kwa karibu suala la kutekwa mfanya biashara Mo Dewji.”

Mbunge mwingine ni, Zitto Kabwe wa kigoma Mjini kupitia Chama cha ACT- Wazalendo ambaye nae amekuwa akiandika mara kwa mara juu ya tukio hilo na maelezo yake akiyaelekeza kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini.

Na Kwa upande wa Chama Cha wananchi CUF upande wa Zanzibar, tukio hilo limemuibua Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya kimataifa ya chama hicho, Ismaili Jussa ameandika "leo ni Siku ya 7. hatuwezi kukaa Kimya.”

Mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyethibitika kuhusika na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo maarufu nchini licha ya jeshi la polisi kuwahoji watu 26.