Ijumaa , 18th Mei , 2018

Shahidi katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchini, Abdul Nondo, amesema kuwa simu ya mtuhumiwa ilikuwa inatumika kipindi alichokuwa anadai kwamba ametekwa.

Shahidi huyo ambaye amejulikana kwa jina la Abdul Kareem anayehusika katika kitengo cha makosa ya mtandao amesema kuwa simu ya Nondo ilikuwa ikitumika katika kipindi ambacho Mtuhumiwa alikuwa akidai ametekwa ingawa ameshindwa kuelezea ilikuwa ikitumika na nani kwa madai kuwa hana uwezo huo.

Akizungumza na www.eatv.tv Wakili wa Abdul Nondo, B. Jebra Kambole amesema kwamba mbali na Shahidi Abdul Kareem, Koplo John ambaye ni mpelelezi katika kesi hiyo ametoa ushahidi wake ambao ni maelezo ya Nondo aliyoyatoa katika kituo cha polisi Iringa.

Wakili Kambole amesema kwamba licha ya serikali kuwa na mashahidi watano katika kesi hiyo, Juni 12-13 inategemea kuwepo na mashahidi wengine ambao bado hawajajulikana watakuwa wangapi.

Hakimu katika kesi hiyo John Mpitanjia ameahirisha kesi hiyo mpaka Juni 12 ambapo Mtuhumiwa Abdul Nondo ataendelea kuwa nje kwa dhamana.

Nondo anatuhumiwa kwa makosa mawili Kosa la kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni Machi 7, 2018 akiwa Ubungo na kusambaza kwa kutumia mtandao wa WhatsApp kuwa yupo hatarini, kosa la pili ni kutoa taarifa za uongo akiwa mjini Mafinga kwa askari Polisi wa kituo cha Mafinga Wilayani Mufindi.