Jumatano , 26th Feb , 2020

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga, amefanya ziara katika Gereza la Wilaya ya Manyoni mkoani Singida na kutoa msamaha pamoja na kuwafutia mashtaka mahabusu 85, ambao walikuwa wakikabiliwa na makosa mbalimbali.

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini DPP Biswalo Mganga

Msamaha huo ameutoa jana Februari 25, 2020 na kusema kuwa mahabusu wengi waliosamehewa makosa yao ni pamoja na wale wa makosa ya uhujumu uchumi, pamoja na wale waliokuwa wanaingia kwenye hifadhi kwa ajili ya kuchimba madini na kukata mbao.

"Baada ya kutafakari na kuangalia mazingira na maslahi ya nchi, nimeweza kufuta kesi za washtakiwa 85 waliokuwa wanakabiliwa na kesi mbalimbali" amesema DPP.

Hatua ya DPP ya kutoa msamaha kwa wafungwa walioko mahabusu ni mwendelezo wa utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli la kuhakikisha mahabusu wanapungua katika Magereza.