Jumanne , 22nd Oct , 2019

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani Kagera, inawashikilia watumishi wanne, akiwamo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa.

Watu wengine wanaoshikiliwa na Taasisi hiyo ni Askari Polisi na Afisa wa
Idara ya Misitu, wote kutoka wilayani Biharamulo.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa TAKUKURU mkoani Kagera, John
Joseph, amesema askari huyo wa Jeshi la wananchi alipokea Shilingi 800,000 kati
ya shilingi milioni 3, alizoomba kutoka kwa mfugaji mmoja, aliyekamata
ng’ombe wake akimtuhumu kuwaingiza katika pori la hifadhi ya Biharamulo.

Aidha Mkuu huyo wa TAKUKURU, amesema kuwa wanamshikilia afisa afya wa Kijiji
cha Nyakanazi, kilichopo katika Wilaya ya Biharamulo, Audastus Norbert kwa
tuhuma za kupokea rushwa ya shilingi elfu 50, ikiwa ni sehemu ya kiasi cha
shilingi laki 2, alichoomba kutoka kwa muuza nyama, baada ya kubaini makosa
katika duka lake.