Jumapili , 20th Oct , 2019

Taasisi Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), inawashikilia watumishi wawili akiwemo Mhasibu wa Hospitali ya Mkoa wa Lindi, Sokoine wakituhumiwa kwa makosa ya ubadhilifu wa fedha za miradi mbalimbali, ukiwemo ujenzi wa wodi ya watoto wenye thamani ya Sh. 221,000,000/-.

Kaimu Mkurugenzi wa taasisi hiyo Brigedia Jenerali John Mbungo aliyaeleza hayo,wakati akizunguzumza na waandishi wa vyombo mbali mbali vya Habari Mjini Lindi amewataja wanaoshikiliwa ni pamoja na Mhasibu wa Hospitali ya Sokoine, Eore Clemence Olomi na Mhandisi msaidizi wa iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama Zebedayo Seleimani.

Brigedia Jenerali Mbungo amesema watumishi hao wanakabiliwa na makosa ya kufanya Ubadhilifu wa Sh,221,000,000/ za Miradi ya ujenzi wa wodi ya watoto, Maabara na Choo kwa matumizi ya wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu.

Amesema makosa yanayowakabili watumishi hao, ni pamoja na kuandaa nyaraka za malipo hewa yanayozidi kiwango kilichoidhinishwa kwenye mikataba iliyoingiwa na wazabuni mbalimbali,huku wakitambua kufanya hivyo ni kosa.

"Uchunguzi wa tuhuma hizi bado unaendelea na pale utakapokamilika tutawajulisheni ndugu zetu waandishi" amesema Jenerali Mbungo.