Tanzania yaahidi kuisaidia Serikali mpya Burundi

Jumamosi , 27th Jun , 2020

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa amesema Tanzania itaendelea kuisaidia Burundi ili ifanikiwe katika adhma yake ya kutaka kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kama ilivyoombwa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza wakati wa uhai wake.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye

Amesema hayo (Ijumaa, Juni 26, 2020) alipozungumza kabla ya mazishi ya Rais Nkurunziza yaliyofanyika kwenye uwanja wa Ingoma uliopo Gitega nchini Burundi, Mheshimiwa Majaliwa amesema ameshiriki mazishi hayo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Marehemu Rais Pierre Nkurunziza alitamani sana kukabidhi madaraka huku akiwa ametimiza kiu yake ya kutaka Burundi iwe mwanachama wa SADC jambo ambalo halikuwezekana naamini Mheshimiwa Rais utalisimamia suala hilo hadi  litimie”, amesema.

Amesema Rais Dkt. Magufuli amemtuma afikishe salamu za pole kwa mke na familia ya marehemu,  Rais wa Burundi  na wananchi wote kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo marehemu Pierre Nkurunziza kilichotokea Juni 9, 2020.

Waziri Mkuu amesema Tanzania  na Burundi ni ndugu na anaamini undugu na mshikamano huo utaendelea kuwepo hata baada ya kifo cha Rais Nkurunziza ambaye alitoa mchango mkubwa katika kuuimarisha mshikamao  huo.

Alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Burundi kumpa ushirikiano Rais wao mpya Evariste Ndayishimiye  kama walivyofanya  kwa marehemu  Nkurunziza ili aweze kuliongoza Taifa hilo vizuri.

Naye, Rais wa Burundi, Ndayishimiye amesema Serikali yake itayaenzi na kuyaendeleza mema yote yaliyofanywa na Marehemu Nkurunziza na aliwashukuru viongozi wote kutoka nje ya nchi yake ambao walishiriki katika mazishi hayo.