Jumatatu , 7th Oct , 2019

Kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2019, thamani ya mauzo ya hisa imefikia Shilingi bilioni 527.41 ambayo ni sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 1,800 ya robo ya pili ya mwaka 2019 na zaidi ya asilimia 1600 ya robo ya tatu ya mwaka 2018.

Soko la hisa

Taarifa hiyo imetolewa leo Oktoba 7, 2019 na Meneja Miradi wa Soko la Hisa la Dar es Salaam(DSE) Emmanuel Nyalali, ambapo amesema kuwa  hisa za Vodacom ndiyo chanzo cha kuongezeka kwa thamani hiyo baada ya wawekezaji wawili wakubwa kuuziana hisa.

''Mpaka sasa kwa mwaka 2019, ni kaunta ya vodacom ndiyo imechangia 85.11 ya thamani ya mauzo ya hisa, ikifuatiwa na TBL kwa asilimia 12.52 na CRDB kwa asilimia 1.69, ambapo kaunta ya Vodacom imechangia kwa asilimia 85.50 ya idadi ya hisa zilizouzwa sokoni, ikifuatiwa na kaunta ya CRDB kwa asilimia 12.93 na TBL asilimia 1.02'', amesema Nyalali.

Kwa sasa thamani ya hatifungani zilizoorodhesha kwenye Soko la Hisa, zilifikia Shilingi trilioni 10.40, ambayo ni sawa na hatifungani za Serikali zenye thamani ya Shilingi  trilioni 10.22 na hatifungani zilizotolewa  na makampuni sawa na thamani ya Shilingi bilioni 176.