Ijumaa , 18th Sep , 2020

Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA), imetolea ufafanuzi wa taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya Kijamii juu ya usalama na ubora wa dawa za sindano zenye kiambata hai chenye jina la 'Remdesivir' zinazotumika kutibu ugonjwa wa COVID-19.

Kwa mujibu wa taarifa ya TMDA kwa vyombo vya habari leo Septemba 18, imeeleza kuwa hivi karibuni kumekuwa na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikihusisha dawa hizo zenye kiambata hai zinajulikana kwa majina ya kibiashara (brand names) kama Covifor.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa, Covifor inayotengenezwa na kampuni yenye jina Hetero Labs Ltd iliyoko nchini India na Jubi-R inayotengenezwa na Jubilant Generics Ltd, India.

"Dawa hizi za sindano zimefungashwa (packed) kwenye vifungashio ambavyo lebo zake zinaonesha haziruhusiwi kusambazwa kwenye nchi za Marekani, Canada na Umoja wa Ulaya (Not for distribution in US, Canada and EU).

Maandishi haya kwenye lebo za dawa hizi yameleta taharuki na wasiwasi kwamba inawezekana dawa zinazosambazwa maeneo mengine ya dunia si salama au ni duni (sub-standard) na hazifai kwa matumizi ya binadamu, 

TMDA inapenda kutoa ufafanuzi kwamba uandishi wa maneno hayo kwenye lebo za dawa hizo ni wa kawaida kwenye sekta ya dawa na lengo lake ni kuzuia usambazaji wa dawa kwenye nchi ambazo mtengenezaji au mgunduzi wa kwanza (innovator company) hajaruhusu kutokana na kuweka haki miliki (patent) ya dawa yake." Ilieleza taarifa hiyo ya TMDA. 

Taarifa hiyo pia ilibainisha kuwa, Dawa hiyo ya Redemsivir imegunduliwa kwa mara ya kwanza na kampuni yenye jina Gilead Ltd iliyoko nchini Marekani na imesajiliwa kwa dharura na Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa na Chakula ya nchini Marekani (US-FDA) kwa ajili ya kutibu COVID-19 (Emergency Use Authorization – EUA).