"Tukimkuta mtu hana kitambulisho ni kosa" - Mwanri

Jumapili , 10th Feb , 2019

Mkuu wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri, amewataka wakuu wa Wilaya waliopo ndani ya mkoa huo kuhakikisha wanagawa vitambulisho vya wajasiriamali na kuwahimiza watu wengi zaidi kuchukua, wasipofanya hivyo basi wawatambue watu hao kuwa ni wavunjifu wa sheria.

Mwanri ametoa kauli hiyo alipokuwa akigawa vitambulisho vya wajasiriamali kwa wakuu wa wilaya mkoani humo, na kuwahimiza kwamba ni lazima wahakikishe wanawahimiza wahusika kuchukua.

Amewataka wakuu hao wa Wilaya kuwatafuta watu wasio navyo na kuwahoji wanafanya shughuli gani mjini, kwani watu wasiokuwa na shughuli yoyote huenda ndio watu wanaouvunja sheria na kuwaibia wengine.

Wapo watu watakaokwambia sina kazi, kataa mwambie hapa kazi tu, huna kazi kosa la pili, la kwanza nimekukuta huna kitambulisho, la pili umesema huna kazi, unaishi ishije, unakula wapi unalala wapi hapa mjini, tunataka uchukue kitambulisho, ili uende ukabangaize kwa ajili ya kutafuta chakula kwa watoto wako, uweze kupata nguo kwa ajili ya watoto wako”, amesema Mwanri.

Mwanri ameendelea kusema, “kwa hiyo tukimkuta mtu hapa mjini hana kitambulisho ni kielelezo kwamba hana shughuli yoyote ni kosa lingine, unambana, unamkuta hashughuliki lakini kavaa vuzuri, tunamuuliza unapata wapi mapato yako, tunajua huyu anaweza akawa muhujumu uchumi, au anapita nyumba za watu. Huna kitambulisho, hufanyi kazi, unaishi vizuri ni kosa lingine, unabambika makosa mpaka, wewe unaishi hapa mjini mtaa mmoja adi mwingine unadoea, kosa lingine, makosa karibu matano hapo”.

RC huyo pia amewasisitiza Wakuu hao wa Wilaya kuhakikisha fedha za kodi kwa wale wafanya biashara wasio na vitambulisho zinakusanywa ipasavyo, kwani wao ndio wawakilishi wa serikali kwenye maeneo yao.