Ijumaa , 14th Jun , 2019

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe, Dkt Balozi Augustine Mahiga, amepokea ripoti ya mapendekezo ya sheria yaliyowasilishwa na Tume ya Kurekebisha Sheria hii leo Juni 14, 2019, Jijini Dodoma.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe, Dkt Balozi Augustine Mahiga.

Akipokea taarifa hiyo Mhe, Dkt Balozi Mahiga amefurahishwa kwa kazi nzuri iliyofanywa na Tume hiyo pamoja na wadau mbalimbali waliofanikisha kukamilika kwa mapendekezo ya sheria ya Ufilisi na nyingine zilizowasilishwa katika tume hiyo  ambazo ni sheria ya Ushahidi na ile ya Mamlaka ya Hifadhi ya  Ngorongoro.

‘’Nimeridhishwa kwa kazi nzuri iliyofanyika kwani tunakwenda kupata sheria madhubuti itakayoendana na hali ya sasa na kusimamia kikamilifu misingi ya utawala bora’’. Alisema Balozi Mahiga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Mhe, Januari  Msofe amesema kuwa tume yake imefanya mapitio na utafiti wa kina kuhusu mifumo ya  Sheria zinazosimamia Ufilisi na kubaini mapungufu ya kisheria na kiutendaji ambao umeathili utekelezaji wa masuala ya hayo hapa Nchini.

Amebainisha mapungufu kuwa ni pamoja na kuwepo kwa sheria mbalimbali za kisekta kama vile sheria ya Makampuni sura ya 212, sheria ya mabenki na taasisi za kifedha sura ya 342 , sheria ya vyama vya ushirika sura ya 211, Sheria ya bima sura ya 394, sheria ya mashirika ya umma Sura ya 57  na sheria ya usajili wa wadhamini sura ya 318 na hivyo kukosekana kwa sheria mahsusi inayosimamia jukumu la ufilisi pekee.

Aidha imeelezwa kuwepo kwa sheria hizo kumesababisha matatizo kwa wadai kutojua taratibu za kupata haki zao kwa wakati pamoja na kuwepo kwa taratibu ndefu zinazochelewesha mashauri ya ufilisi kumalizika kwa wakati mara baada ya taasisi au kampuni husika kufilisika.