Jumatano , 18th Oct , 2017

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya, IEBC, Wafula Chebukati, amewashutumu wanasiasa nchini humo kwa kutatiza maandalizi ya uchaguzi wa marudio wa rais unaotarajiwa kufanyika Alhamisi wiki ijayo.

Bw. Chebukati amesema maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vyema lakini katika mazingira ya sasa ni vigumu kuandaa uchaguzi huru na wa haki iwapo hakutakuwa na mabadiliko.

Amesema, maafisa wakuu kwenye tume ya uchaguzi ambao wametajwa kwa njia moja au nyingine kwamba walihusika katika kuvuruga uchaguzi wa kwanza tarehe 8 Agosti wanafaa kujiuzulu.

Bw Chebukati amesema hayo saa chache baada ya mmoja wa makamishna wa tume hiyo Dk. Roselyn Akombe kutangaza kujiuzulu akiwa Marekani na kusema hana mipango yoyote ya kurejea Kenya hivi karibuni.