Jumapili , 12th Aug , 2018

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni amekabidhi mashine 10 za kufyatulia matofali kwa Jeshi la Magereza la mkoa wa Lindi na kuwataka kuzitumia ipasavyo ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili ikiwemo makazi duni.

Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Rajabu Nyange, akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati), baada ya kupokea mashine 10 za kufyatulia tofali ambapo ni mpango maalumu wa serikali kuondoa changamoto za makazi ya askari magereza nchini. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi,Shaibu Ndemanga.

Mashine hizo ni sehemu ya ahadi aliyoitoa mwaka mmoja na nusu uliopita baada ya kufanya ziara katika mkoa huo na kukutana na changamoto mbalimbali ikiwemo makazi duni ya nyumba za udongo hasa katika gereza la Lindi mjini.

Aidha, Mhandisi Masauni amewataka wakuu wa Jeshi la Magereza mkoani humo kujipanga ipasavyo namna ya kuzitumia machine hizo ili ziwe na tija na manufaa kwao.

"Nawakabidhi mashine hizi, natarajia kuona mabadiliko yenye tija kutoka kwenu, mkifanya vizuri nitawatafuta wadau wengine kwa ajili ya kuongeza mashine hizi. Nataka gereza la Lindi Mjini liwe la mfano kwa magereza ya mkoa huu. Tumieni nguvu kazi ya wafungwa mlionao kwa ajili ya kuboresha makazi yenu", amesema Masauni.

Hata hivyo, Masauni amesema ana matumaini makubwa na magereza katika kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuzitumia mashine hizo kwa ufanisi mkubwa ili wapate makazi bora kwa manufaa ya askari na maofisa wao.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza ya Mkoa wa Lindi (RPO), Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Rajab Nyange amemshukuru Mhandisi Masauni kwa msaada huo alioutoa kwa kile alichokielezea kuwa hali ya makazi ya askari wa jeshi hilo siyo nzuri

Naye, Mkuu wa gereza la Lindi Mjini (SP), Emanuel Pagali amesema mashine hizo ni nzuri na zitawasaidia kwa utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kuboresha makazi ya maofisa na askari wa jeshi hilo