Jumapili , 14th Oct , 2018

Rasi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt Ali Mohamed Shein amezitaja sifa tatu za hayati Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wake ambazo zimepelekea mpaka sasa Tanzania kuendelea kuenzi fikra za kiongozi huyo.

Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, Dkt Ali Mohamed Shein

Dkt Shein amezitaja sifa  hizo akiwa mkoani Tanga wakati wa mahitimisho ya kilele cha miaka 19 ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, kilele cha maadhimisho ya mwenge wa uhuru na kufunga kwa wiki ya vijana kitaifa mkoani humo.

Miongoni mwa sifa alizozitaja Dkt Shein ni pamoja na mwalimu alikuwa ni kiongozi anayependa Umoja na Mshikamano.

Amesema kiongozi huyo alikuwa muumini mzuri wa ujamaa na mshikamano wa pamoja kulikopelekea kuzalishwa kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Mzalendo, amesema sifa nyingine iliyokuwa kwa kiongozi huyo muasisi wa taifa ni kuwa mtu mwenye uchungu na taifa lake kwa kuhamasisha watanzania kuenzi tamaduni za asili.

Mwanafalsafa, aidha pia Dkt Shein amesema watanzania hatuna budi kumuenzi kwa sababu ameacha falsafa ambazo zinaisaidia Tanzania kwa sasa na miaka mingi ijayo.

"Mwalimu Nyerere alionesha namna alivyotaka tuwe wazalendo na taifa letu, hivyo kila wakati tunapomkumbuka Mwalimu, lazima tuyakumbuke na tuyapende yaliyo yetu kwa kuthamini kilicho chako na kusahau cha mwenzako", amesema Dkt Shein.

Akitaja mafanikio ya mbio za mwenge mwaka huu, Dkt Sheinamesema,"mbio za mwenge zinatupa fursa kwa nchi yetu kidiplomasia na mataifa ya nje kutokana na historia yetu ya kupigania uhuru wa mataifa ya nje, na inaambatana na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo kwa miaka 3 imezindua miradi 1414 yenye thamani ya bilioni 67".

Kuhusiana na suala la vijana Dkt amesema, "serikali zetu mbili tutaendelea kuboresha elimu bora kwa vijana na kuhamasisha ubunifu, ili kupunguza tatizo la  ajira kwa vijana, tutandelea kuwahimiza wadau kuwekeza kwenye elimu".