Jumatatu , 19th Aug , 2019

Hatimaye wananchi  wa Kipunguni waliopisha upanuzi wa Jengo la tatu la Abiria katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,  wameanza kugawiwa maeneo yao hii ni baada ya kuwepo kwa mgogoro wa makubaliano kati ya kampuni ya kupima viwanja ya Tanzania Remix na wamiliki halali.

Moja ya majengo Terminal

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye, wakati akizungumza na EATV & Radio Digital na kusema kuwa, hadi sasa takribani viwanja zaidi ya 400 vilivyopo kata ya Msongola  vimekwishagawiwa.

''Sisi Tanzania Remix walitupatia baadhi ya viwanja na  bado tunawadai vichache sana na wako kwenye taratibu za mwisho za kuhakikisha,  hivyo vichache vilivyobakia kati ya 537 vinakamilika ili wananchi wale waliopisha upanuzi wa kiwanja cha ndege waweze kupatiwa viwanja vyao'',  amesema Naibu Waziri.

Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), imekwishailipa Kampuni ya Tanzania Remix kiasi cha shilingi bilioni 3.7 kwa ajili ya viwanja 537,  vitakavyolipwa fidia kwa wananchi wa Kipunguni na Kigilagila waliopisha mradi huo.