Ijumaa , 10th Aug , 2018

Uingereza imetoa msaada wa shilingi Bilioni 307.5 kwa Tanzania kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika elimu, mapambano dhidi ya rushwa na uboreshaji huduma za afya.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuonesha albamu ya picha Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza Mhe. Penny Mordaunt inayoonesha Shule ya Sekondari ya Ihungo iliyobomolewa kabisa na tetemeko la Ardhi mkoani Kagera lililotokea Septemba 10, 2016 ambayo imejengwa upya na serikali ya Uingereza kupitia mpango wake wa maendelo ya elimu kupitia UKAid/DFID.

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza Mhe. Penny Mordaunt ametangaza msaada huo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Penny Mordaunt amesema fedha hizo zinatolewa kwa ajili ya kuunga mkono vipaumbele vya Rais Magufuli ambapo kati yake shilingi bilioni 124.5 zitaelekezwa katika kuinua ubora wa elimu hususani kutoa fursa ya elimu kwa watoto wa kike na wenye ulemavu, shilingi Bilioni 23.5 zitaelekezwa katika kuunga mkono juhudi za kupambana na rushwa, na shilingi bilioni 160 zitaelekezwa katika kuboresha huduma za afya.

Tunafanya hivi ili kudhihirisha dhamira yetu ya kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wetu, tunataka kujielekeza katika kuhakikisha Rais Magufuli anafanikisha ahadi zake kwa Watanzania na tunafurahi kuwa wadau muhimu wa hilo amesema Mordaunt.

Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Penny Mordaunt kwa msaada huo na amemuomba kufikisha shukrani zake kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Theresa May kwa mchango mkubwa ambao Uingereza hutoa kuchangia bajeti ya Serikali na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo huku akimkabidhi albamu ya picha za shule ya sekondari Ihungo mkoani Kagera iliyojengwa upya baada ya kuharibika kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 2016 ambapo shilingi Bilioni 6 zilizotumika kujenga majengo hayo zilitolewa na ubalozi huo.