Jumapili , 18th Dec , 2022

Waziri wa Nishati January Makamba, amesema kuwa hadi mwezi Novemba 2022, ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) umefikia asilimia 78.68, na  mradi huo una hatua kubwa mbili ambazo zina hadhi ya kushuhudiwa na kusheherekewa.

Waziri wa Nishati January Makamba

Waziri Makamba amezitaja hatua hizo kuwa ni kufunga lango la njia ya mchepusho wa maji na ya pili ni kuwasha mitambo ya kufua umeme.

"Tunategemea itachukua misimu miwili ya mvua kulijaza bwawa na kuanza kujaribu mitambo, bwawa la Mwalimu Nyerere linahifadhi lita 33.2 bilioni za maji na kama zikitumika na mitambo yote itaweza kuendesha mitambo kwa kipindi cha mwaka mmoja," amesema Waziri Makamba.

Aidha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio la kushuhudia ufungaji wa lango la handaki mchepuko (yaani diversion tunnel) ili kuruhusu maji yaanze kujaa katika bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere litakalofanyika Desemba 22,2022.