Jumamosi , 13th Jul , 2019

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, ameungana na wananchi wengine wa Chato,wakiwemo viongozi wa Serikali na mabalozi, kwa pamoja kumpokea Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, katika uwanja wa Ndege wa Chato aliyekuja kwa ziara binafsi ya siku moja.

Rais Magufuli

Kwa pamoja wakati wakizungumza na wananchi waliofika katika mapokezi hayo, wameendelea kusisitiza undugu, umoja na ushirikiano katika masuala ya biashara, na utendaji kazi ili kuweza kukuza uchumi wa nchi hizo, na wananchi wake kuongeza vipato.

Katika hotuba yake Rais wa Uganda Yoweri Museveni, ameendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kufanya kazi, badala ya kutegemea ajira za serikali ambazo kiuhalisia hazitoshi.

Aidha Rais Magufuli, amempongeza mgeni wake huyo kwa kuendelea kujitoa kwa ajili ya watanzania, waliopigana na kumwaga damu kwa ajili ya nchi hiyo, kujikomboa katika vita dhidi ya Nduli Idd - Amin Dada.

''Ni binadamu wachache sana wanaokumbuka walikotoka hasa wanasiasa, umetukumbusha sisi wanasiasa , nakumbuka pia tetemeko la Bukoba ulitusaidia kwenye  Mv Nyerere ulikuwa wa kwanza pia, hii inaonyesha ni namna gani umekuwa ndugu yetu'' amesema  Rais Magufuli.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni, ni Rais wa pili sasa kufika Chato, kwa ajili ya ziara binafsi na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli, baada ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kufungua njia Julai 5, 2019.