Alhamisi , 12th Jan , 2017

Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuhakikisha usalama wa Zanzibar unaimarika na kuboresha ushirikiano wa kidemokrasia uliopo baina ya Zanzibar na Tanzania Bara ili kuheshimu utu na kutekeleza malengo yaliyowekwa na waasisi wa taifa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Dkt. Augustine Mahiga.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga kwenye mazungumzo na EATV ilipohoji kuhusu mchango wa Tanzania Bara katika kuleta maendeleo ya visiwani Zanzibar ikiwa leo inaadhimisha miaka 53 ya kumbukumbu ya mapinduzi yake matukufu.

Amesema muungano wa Zanzibar na Tanganyika umedumu kwa sababu kumekuwa na manufaa ambayo yanakidhi mahitaji ya wananchi wa pande zote.

Amesema wizara yake inatekeleza na kusimamia muungano kwa kuhakikisha kwamba misaada yote ambayo inapatikana kimataifa inakwenda pande zote mbili za Tanzania na wanaendelea kuimarisha mfumo huo kwa kuheshimu katiba za pande zote mbili zilizopo.