Uuaji, ubakaji na uporaji vyaogopesha Kimara

Ijumaa , 14th Sep , 2018

Wakazi wa maeneo ya Kimara jijini Dar es salaam wameingiwa na hofu kwa madai ya matukio mbalimbali ya uporaji, ubakaji, na mauaji yanayotokea katika maeneo yao hususani nyakati za usiku na kulitaka jeshi la polisi kuweka ulinzi mkali katika maeneo yao.

Picha haihusiani na tukio.

Wakizungumza katika kipindi cha East Africa Breakfast kinachorushwa na East Africa Radio, wakazi hao wawesema matukio hayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara hususani maeneo ya Suka (Kimara) ambapo matukio ya mauaji na ubakaji yamekuwa yakishamiri huku yakiwaacha na hofu kubwa na kuwalazimu kuwahi kurudi nyakati za usiku.

Hapa mpaka sasa nimesikia matukio mawili yametokea na mengi ni nyakati za usiku, hali imekuwa ni tete. Kuna mtu amekutwa amefariki haijulikani kama amepigwa au la, na kuuawa maeneo ya Suka, na lingine kuna mama alibakwa nyakati za usiku huko huko Suka. Yaani hatujui ni kwanini matukio yamekuwa yakitokea, yanatunyima raha sana”, amesema mkazi mmoja wa Kimara.  (Jina limehifadhiwa)

Mkazi mwingine wa eneo hilo naye akazungumza, "Watu wanabakwa na kuuawa,ikifika muda tunarudi mapema nyumbani hatutaki tabu, mi mwenyewe nakunywa pombe lakini ikifika saa mbili nipo nyumbani, hata kama sina kitu ni bora nirudi nyumbani. Nisije kupigwa nondo na watu wenyewe wanaonekana sio wakazi wa huku,ukitembea usiku ukimuona mtu unakuwa na hofu"

Akizungumzia suala hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni ACP Murilo Jumanne, amekiri kutokea kwa tukio moja kubwa hususani ya unyang'aji kwa kutumia silaha na mtu kupigwa nondo na tayari Jeshi la polisi limeshachukua hatua stahiki kwa watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani.

Aidha Kamanda Murilo amekataa kuwataja ni watuhumiwa wangapi wamekamatwa mpaka sasa kwani anasema kufanya hivyo kutawapa taarifa watuhumiwa juu ya mambo yanayoendelea ndani ya jeshi hilo.

Tathimini mbalimbali zilizotoka ndani ya jeshi la polisi kuhusiana na matukio ya uhalifu nchini inaonesha takribani matukio yaliyoripotiwa kwa mwaka 2017 ni pamoja na makosa ya unyang'anyaji wa kutumia silaha 127, ulawiti 48, unyang'anyaji wa kutumia nguvu 838 na uvunjaji 3,695, yakihusisha matukio ya vijana wa panyarodi na mauaji ya kibiti.

Msikilize hapo chini Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni ACP Murilo Jumanne akizungumzia matukio hayo.