Jumatano , 16th Mei , 2018

Zikiwa zimepita takribani siku 6 tokea kulipofunguliwa dirisha la uombaji mikopo kwa njia ya mtandao nchini, wanafunzi na wadau mbalimbali wameendelea kuilalamikia Bodi ya Mikopo kwa kuweka vigezo vigumu bila ya kuwafikilia kwa undani watu wanaotaka kufaidika nayo.

Akizungumza kwenye kipindi cha EATV Saa1 Katibu Mtandao wa Wanafunzi nchini (TSNP), Joseph Malecela amesema katika utoaji wa mikopo hiyo kumekuwa na ubaguzi wa upendeleo kwa baadhi ya michepuo ya wanafunzi hasa hasa wanaosomea sayansi huku wengine wakikosa kabisa.

Mbali na hilo, Malecela amesema ni vyema Bodi ya Mikopo itoe ufafanuzi zaidi juu ya kifungu cha muongozo wa kuomba Mkopo Na 1.0 (vii) ambacho kinasema 'waombaji ambao wazazi au walezi ni wamiliki wa biashara, mameneja wakubwa katika mamlaka zinazotambulika zenje usajili, hawaruhusiwi kuomba mkopo'.

"Sisi tunachojiuliza kama Mtandao wa wanafunzi Tanzania kwamba tuna mfumo gani wa mkopo ambao unaweza kupima kiwango cha uwezo wa mzazi katika kuweza kumudu hizo gharama, na madodoso gani yamewekwa ili kujua huyu mtu anafanya biashara kubwa hata kama si Meneja mkubwa", amesema Malecela.

Kwa upande wake Afisa Mawasiliano Mwandamizi kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Bi. Veneranda Malima amesema kifungu hicho kipo sawa na hawawezi kusema kwamba kitaondolewa.

Sikilize hapa chini mjadala mzima kupata kufahamu maana halisi ya kigezo cha leseni kilichoweza kuzua gumzo kila mahali.