Viongozi wa CHADEMA na wafuasi washikiliwa polisi

Jumanne , 13th Mar , 2018

Diwani wa Kata ya Mabatini, Deo Mbibo pamoja na watu takribani 20 wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CHADEMA wanashikiliwa na polisi baada ya kukamatwa walipokuwa wameenda kuhani msiba wa mwanachama mwenzao.

Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mwanza, Leonard Nundi amesema tukio hilo limetokea leo Machi 13, saa kumi jioni ambapo wafuasi hao wakiwa zaidi ya 500 walienda kuhani msiba huo na ghafla polisi waliwavamia na kumtaka mfiwa kuongea naye.

“Chanzo cha vurugu ni baada ya askari hao kuvamia msibani na kumhitaji mfiwa ambaye ni Laurent Chiro kwa ajili ya mazungumzo, waliposhindwa kuelewana walimchukua diwani na viongozi wengine waliokuwa meza kuu na kuwapandisha kwenye gari la polisi,” amesema Nundi.

Amefafanua kwamba wanachama waliokuwa msibani waliogomea kitendo hicho na kuanza kuwarushia mawe polisi ambao nao walijihami kwa kupiga mabomu ili kuwatawanya.