Jumamosi , 8th Dec , 2018

Wabunge wanaotoka Vyama vya Upinzani nchini wametakiwa kufuata sheria na taratibu pindi wanapoenda kwenye vikao vya Bunge Jijini Dodoma, na wala wasifanye shughuli ambazo zitapelekea kutiwa nguvuni na vyombo vya dola.

Wabunge wa upinzani wakiwa wamegoma

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobasi Katambi kwenye mahojiano yake maalum na www.eatv.tv aliyofanya hivi karibuni.

Katambi amebainisha kuwa hajawahi kukutana na wabunge wa upinzani pindi wanapokuja kwenye vikao vya bunge Jijini Dodoma, lakini amewaahidi atawashughulikia endapo watafanya makosa ambayo wamekuwa wakifanya sehemu nyingine.

"Mimi sijawahi kukutana na mbunge yeyote wa upinzani lakini kila wanapokuja Dodoma lazima wafuate sheria, na taratibu za nchi kwa sababu Dodoma ni makao makuu ya nchi, serikali na chama kinachoongoza dola kwa hiyo wanapokuwa hapa wafanye kazi za kibunge na si vitu vingine kwa sababu watakuwa chini yangu kama Mkuu wa wilaya." Amesema Katambi.

Akijibu swali juu ya kauli hiyo hadhani inalenga kuwatisha wabunge wa upinzani Katambi amesema  "siwatishi na wala simtishi mtu yeyote awe mbunge au mtanzania yeyote waje tu lakini lazima akifika Dodoma afuate sheria, na aoneshe uzalendo anapokuwa Dodoma."

Mapema wiki hii Mkuu huyo wa Wilaya aliweka masharti ya kuelewana na Mwenyekiti wake wa zamani Freeman Mbowe kuwa lazima ajipambanue kuwa ni mtu ambaye anaunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali.

Katambi pia alikanusha madai ya kufanya udhalilishaji kwa baadhi ya watuhumiwa ambao amekuwa akiwakamata na kuwaonesha kwenye vyombo vya habari.