Jumatano , 16th Mei , 2018

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), Patrick Ole Sosopi, amesema Wabunge wa CHADEMA kutolewa Bungeni sio kwasababu ya mapungufu yao bali ni uimara na uwezo wao wa kujenga hoja.

Sosopi ameyaeleza hayo leo kwenye kipindi cha KIKAANGONI kinachoruka kupitia Ukurasa wa 'Facebook' wa East Africa Television, wakati akijibu swali la mtazamaji juu ya wabunge wa chama chake kutojenga hoja na kuchangia Bungeni kama zamani.

''Tanzania kwasasa tunakumbana na tamaduni mpya ya kisiasa, kwahiyo kutoona wabunge wa CHADEMA wakichangia sio kosa lao, nimpe pole tu mtazamaji kwasababu haoni 'Bunge Live' mana halioneshwi ila wabunge wako imara'', amesema.

Mwenyekiti huyo amewatolewa mfano Mbunge wa Kibamba John Mnyika na Ester Bulaya wa Bunda, kuwa wameonesha uimara na uwezo wao ndio mana wameondolewa Bungeni hivi karibuni kwasababu watawala wanataka kusikia mazuri tu.

Sosopi ameongeza kuwa wanatamani kuona uhuru wa kufanya siasa ukiendelea kama ilivyokuwa zamani na sio kusubiri hadi wakati wa uchaguzi mwaka 2020 ndio wafanye mikutano ya kisiasa.