Wadada wa kazi kulipwa zaidi ya laki mbili

Wednesday , 13th Sep , 2017

Serikali ya Namibia imetangaza nyongeza ya mishahara ya watumishi wa ndani kwa 11%, pamoja na marekebisho ya masharti ya ajira ambayo itaanza kutumika kuanzia Oktoba Mosi mwaka huu.

Aidha serikali imewataka watu wote walioajiri watumishi wa ndani kujisajili katika Wizara ya Kazi na Ajira ya nchi hiyo hadi Novemba 30.

Sasa mshahara mpya wa mwezi kwa watumishi wa ndani utakuwa Dola ya Namibia 1,502.05 ambayo ni zaidi ya laki mbili na nusu fedha ya Tanzania wakati mshahara wa wiki na siku utakuwa Dola ya Namibia 346.89 na Dola 69.37.

Aidha, watumishi wa ndani wasioajiriwa moja kwa moja watakuwa na uhakika wa kulipwa mshahara sawa na saa tano za kazi kwa siku.

Serikali imesema, umuhimu wa watumishi wa ndani kamwe hauwezi kupuuzwa kwani wanachangia katika kuhakikisha matunzo ya familia na pia kwa uchumi wa nchi.

Namibia iliunda Tume ya Mishahara ya Watumishi wa Ndani mwaka 2012 kwa lengo la kuhakikisha watumishi hao wanalipwa mishahara stahiki na haki zao nyingine na waajiri wao.