Jumapili , 20th Sep , 2020

Katika kuhakisha uwepo wa ushiriki wenye tija kiuchumi taasisi na mashirika yametakiwa kuweka mikakati ya kukutana ili kujenga ushirikiano pamoja na kubadilishana ujuzi ili kuendeleza huduma mbalimbali wanazotoa.

Watangazaji wa East Africa Television na East Africa Radio, Donald Mtani, Tigana Lukinja na Ibra Kasuga wakiwa na zawadi baada ya kumaliza MasakiCorporateRun zilizofanyika uwanja wa Farasi, Oysterbay Jijini Dar es Salaam.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na washiriki mbio za Serengeti Lite Masaki Corporate ambazo zimekutanisha wadau wa kampuni mbalimbali ambapo licha ya mbio hizo kuimarisha afya iwapo zitaratibiwa mara kwa mara zinaweza zikaongeza tija katika uchumi wa nchi.

Kwa upande wake mjumbe wa kamati tendaji kutoka chama cha riadha na kocha wa riadha Idd Muhunzi amepongeza mkakati huo huku akiwataka waanzishaji wengine kuendelea kufuata sheria za usajili ili kusaidia kupatikana wakimbiaji bora ambao watashindanishwa katika matukio ya kitaifa.

Kwa upande wao wajasiriamali walioshiriki katika kuonesha na kuuza bidhaa zao katika tukio hilo wamesema ni fursa nzuri kwao kwani wanapata nafasi ya kukutana na wateja wao

"Ukweli ni kwamba hizi sio riadha tu ni fursa kubwa ya uwekezaji hapa na ni muhimu kila mwekezaji akaona thamani yake inapanda haswa baada ya kukutana na wadau na kufanya mahusiano ya kibiashara na kuendeleza shughuli zao kwa kuzingatia taratibu za sheria"Alisema Peace Robert ambaye ni mjasiriamali.

Mbio hizo zilizoshirikisha mbio za miguu na baiskeli zilidhaminiwa pia na East Africa Radio, ambapo baadhi ya watangazaji wa East Africa Radio na East Africa Television walishiriki.