Jumatano , 5th Dec , 2018

Kutokana na malalamiko ya wafanyabiashara wa nchi za Zambia na Malawi kutopatiwa risiti na wafanyabiashara wa Tanzania, serikali mkoani Songwe imewapa wafanyabiashara hao siku 4 kununua mashine za lisiti za EFD kuanzia wiki ijayo na atakayebainika hana mashine hiyo atachukuliwa hatua.

Meneja wa TRA Mkoa wa Songwe, Paul Walalaze ametoa agizo hilo baada ya kuwatembelea wafanyabiashara wa soko la Manzese lililopo katika mji wa Tunduma mkoani humo na kubaini wafanyabiashara wa soko hilo wanatumia vitabu vya risiti  badala ya mashine za kieletroniki.

Meneja amesema kuwa taarifa hizo wamezipata kutoka nchi jirani ya Zambia na Malawi ambapo wafanyabiashara wamekuwa wakipewa risiti feki.

www.eatv.tv imefika katika soko hilo na kuzungumza na baadhi ya wafanyabiashara  ambao wamepongeza hatua ya viongozi wa mapato kuwatembelea na kuwapa elimu huku wakiomba elimu hiyo isiishie Tunduma badala yake iwafikie na maeneo mengine.

Wakati huohuo mamlaka ya mapato TRA Mkoa wa Songwe imeongoza kitaifa kwa ukusanyaji mapato, ikiwa imevuka lengo walilokuwa wamepangiwa.