Jumatatu , 8th Jul , 2019

Watu 7 wamefariki dunia na watatu wamejeruhiwa, katika ajali iliyotokea eneo la Malendi Iramba mkoani Singida. 

Picha ya ajali

Taarifa zinaeleza kuwa watu hao ni waandishi wa habari waliokuwa katika safari ya kikazi, wakielekea Chato mkoani Geita. Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi, Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Tabora.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, ambapo gari dogo walilokuwa wamepanda wafanyakazi hao limegongana na lori lililokuwa likitoka Igunga kuelekea Dar es salaam.

Miongoni mwa vifo hivyo ni pamoja na wafanyakazi wa Azam Media, Salim Mhando, Florence Ndibalema, Said Haji, Sylvanus Kasongo na Charles Wandwi, wengine ni dereva na utingo wake ambao majina yao hayajafahamika.

Majeruhi ni Mohamed Mwinshehe, Mohamed Mainde ambao wapo ICU pamoja na Artus Masawe ambaye yake ni nzuri kiasi.

Kufuatia taarifa ya ajali hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ametoa salamu za rambi rambi kwa uongozi na wafanyakazi wa Azam Media kwa kupoteza wafanyakazi wake watano.

"Nimeshtushwa sana na vifo hivi, nampa pole Mwenyekiti Ndugu. Said Salim Bakhresa, ndugu wa marehemu wote, Mtendaji Mkuu Ndugu. Tido Muhando na wafanyakazi wote wa Azam Media Ltd, waandishi wa habari wote na watu wote walioguswa na vifo hivi", amesema Rais Magufuli katika taarifa rasmi ya Ikulu.