Jumanne , 9th Jul , 2019

Miili ya waliyokuwa wafanyakazi wa Azam Media ambao walifariki kwa ajali asubuhi ya Julai 8, 2019 eneo la Malendi Iramba mkoani Singida, inatarajiwa kuagwa leo katika makao makuu ya ofisi za Azam Media zilizopo Tabata jijini Dar es salaam.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Azam Media Yahya Mohamed amesema kwa sasa taratibu za utambuzi wa miili kwa ndugu bado zinaendelea, na baada ya hapo shughuli za kidini zitafuata ambapo, marehemu ambao ni Waislamu watapelekewa msikitini, na Wakristo wataelekea makao makuu ya Azam, kwa ajili ya kuagwa.

"Taratibu zinazoendelea ni kuandaa miili na tayari tumeshaandaa miili ya miwili, tukishamaliza miili yote tutaelekea ofisini Tabata, kupitia barabara ya Jangwani na kupita njia ya Kigogo, pale ofisini kutakuwa na shughuli maalum ya kuwaaga na kuwakabidhi ndugu zetu kwa familia zao." amesema Yahya Mohamed

"Tunaomba ndugu zetu Watanzania mjitokeze kushiriki mazishi pindi miili itakapokabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za mazishi" amesema Yahya Mohamed

Miongoni mwa waliofariki kwenye ajali hiyo, Salim Mhando, Florence Ndibalema, Said Haji, Sylvanus Kasongo na Charles Wandwi.