Jumanne , 22nd Mei , 2018

Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Saada Ramadhan Mwandwa ameitaka serikali kuweka utaratibu wa kuwatenganisha wafungwa wa makosa ya ubakaji wakiwa gerezani ili kuwanusuru watu hao kutoendelea na tabia hizo wakiwa kwenye kifungo.

Mjumbe huyo ameyasema hayo wakati akiuliza swali lake la msingi katika kikao hicho na kuhoji kuwa serikali haioni kwamba kuwachanganya wafungwa wa makosa mengine kunaweza kuwafanya kuendelea na tabia ya ubakaji wakiwa kifungoni.

Akijibu swali la mwakilishi huyo wa nafasi za wanawake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum, Shamata Shaame Khamis amesema kuwa hakuna maeneo maalum gerezani yanayotengwa kwa ajili ya kuwekwa makundi fulani ya wahalifu wanaotumikia adhabu zao.

"Wanaotumikia adhabu wakiwa gerezani wanaweza kuhukumiwa kutokana na makosa tofauti yakiwemo uhaini, wizi, ugaidi, unyang'anyi pamoja na hayo ya ubakaji na udhalilishaji wa wanawake pamoja na Watoto. Ni kweli kila kosa linaathari zake kisailolojia kwa mkosaji na kwa wale wanaomzunguka", amesema Shaame.

Kwa upande mwingine, Shaame amesema chuo cha mafunzo kina-program ya ushauri nasaha kwa wafungwa hasa wale wafungwa wenye hulka za kipekee kama wa makosa ya ubakaji.