Jumamosi , 9th Nov , 2019

Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama 11 visivyokuwa na wawakilishi bungeni, Abdul Mluya amesema kuwa watu waache kuwabeza kwakuwa wameamua kutosusia zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwamba vyama hivyo tayari vinao wagombea.

Mkutano wa vyama 11 visivyokuwa na wawakilishi bungeni na waandishi wa habari

Kauli hiyo ameitoa leo Novemba 9, 2019, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, ambapo amesema katika umoja wao wapo wagombea ambao hawakukidhi vigezo na majina yao yametolewa kwa kuwa tu hawakujaza taarifa zao vizuri na hivyo nia yao kubwa ni kushiriki uchaguzi huo. 

"Wagombea tunao katika maeneo tofauti ambayo vyama vyote 11 vimepata, sisi hatupati ruzuku na ndio maana hatuwezi kujilinganisha na vyama ambavyo vinapata ruzuku, sisi tukipata hata 5 kwa uwezo wa vyama vyetu bado vinatosha.", amesema Mluya.

"Wenzetu wanafanya hivyo sababu wanaweza kusimamisha wagombea nchi nzima na wakipata wagombea 10 wanaona wamekosa, sisi tunadhani ni bora tupigane tupate ili tuondokane na hizo kauli za hao hao wanaotulalamikia kuwa hatuna wawakilishi pande zote, na huenda wataacha kutuita haya majina machafu wanayotuita.", ameongeza.

Aidha Mluya ametoa wito kwa vyama vilivyojitoa kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kuwa suala la siasa linahitaji mikakati na akili na suala la kujitoa katika uchaguzi haoni kama ni mbinu sahihi badala yake ni kujitia hasara tu.