Jumanne , 29th Sep , 2020

Jeshi la Polisi nchini limesema kuwa litaanza kuchukua hatua kwa wagombea wote ambao hawafuati ratiba ya kampeni iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi jambo ambalo ni kosa kulingana na kanuni za maadili ya vyama vya siasa na uchaguzi.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi Nchini, CP Liberatus Sabas.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi Nchini, CP Liberatus Sabas, leo Septemba 29,jijini Dodoma ambapo amesema kuzingatia ratiba kunasaidia kulinda usalama wa raia na mgombea mwenyewe. 

“Kwa hiyo kuanzia sasa niseme tutaanza kuchukua hatua  kwa sababau usipochukua hatua likitokea lakutokea sisi jeshi la polisi ndio tunaokwenda kulaumiwa kwamba hatukutoa ulinzi ndio maana watu hawa wamedhurika” alisema Kamishana Sabas   

Aidha Kamishna Sabas, amesema kuwa jeshi la polisi limefikia hatua hiyo kutokana na kuwepo kwa baadhi ya wagombea ambao wamekuwa wakifanya kampeni kwenye maeneo ambayo hayako kwenye ratiba ya kampeni.

Katika hatua nyingine jeshi la polisi limelaani vikali vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wagombea na wafuasi wao vyakutoa lugha za matusi, uzushi na uongo pamoja na kashfa kwa wagombea wengine zikiwa na lengo la kupandikiza chuki kwa wananchi.

Jeshi la polisi limetoa rai kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kubaini na kuzuia uhalifu  ili kuzuia kuathiri amani na usalama wa nchi.