Jumamosi , 20th Apr , 2019

Msimamizi wa Uchaguzi katika jimbo la Arumeru Mashariki Emmanuel Mkongo amebainisha sababu ya aliyekuwa Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Dkt. John Palangyo kupita bila kupingwa kwenye uchaguzi wa Jimbo la Arumeru Mashariki, ni kwamba baadhi ya wagombea kutorudisha fomu za kuwania ubunge

Mbunge mteule Dkt John Pallangyo

Akitangaza sababu ya mgombea wa CCM kupita bila kupingwa Mkongo amesema, idadi kubwa ya wagombea walishindwa kufuata taratibu na sheria zinazoongoza kanuni za Uchaguzi wa Urais na Ubunge na Udiwani.

Emmanuel Mkongo amesema kuwa "wagombea watatu hawakuteuliwa kwa sababu hawakurudisha fomu, ambao ni Antonia Ndosi (DP), George Nashoini (CUF), na Msifuni Mwanga (TLP), fomu za wagombea wengine 7 zilirudishwa lakini zilikuwa na mapungufu ya kisheria."

"Mgombea wa SAU hakuteuliwa kwa sababu hakudhaminiwa na wapiga kura 25, na kushindwa kukidhi matakwa ya sheria ya uchaguzi, mgombea huyu pia hakulipa dhamana ya shilingi 50000." ameongeza Mkongo

"Mgombea Tirusbia Joseph wa UPDP mapungufu yake ni kutowasilisha picha kwenye fomu ya kuwania Ubunge, na yeye pia hakulipa gharama ya 50000." amesema Mkongo

April 19, 2019 Msimamizi huyo wa Uchaguzi alimtangaza aliyekuwa Mgombea wa CCM Dkt. John Palangyo kuwa Mbunge mteule wa Jimbo la Arumeru Mashariki na kurithi nafasi ya Joshua Nassari.