Alhamisi , 23rd Apr , 2020

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, amesema kuwa bado hajapata taarifa za waathirika wa Virusi vya Corona, waliopo katika kituo maalum katika Hospitali ya Amana, kama wametoroka na kurejea makwao ila anachojua walikuwa wanatishia kuondoka kwa madai ya kuwa hali zao kiafya ni nzuri.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema.

Mjema ameyabainisha hayo leo Aprili 23,2020, wakati akizungumza na ITV, kufuatia taarifa mbalimbali zilizokuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa, baadhi ya wagonjwa katika hospitali hiyo wameleta vurugu na wengine kutoroka.

"Bado hatuna taarifa ya wagonjwa katika Hospitali ya Amana waliotoroka na kupanda daladala kurejea makwao, ngoja tuifuatilie ila tunachojua ni kwamba walikuwa wanasema wanataka kurudi nyumbani, kifupi walikuwa wanatishia tu" DC Ilala, Sophia Mjema.

Aidha DC Mjema ameongeza kuwa "Kulikuwa na wagonjwa ambao walikuwa wamefika pale na kusema kuwa wao hawaumwi sana kwahiyo walikuwa wanataka waruhusiwe na unajua ukifika pale, ukiwa mshukiwa lazima ukae kidogo hospitali uangaliwe wakuone upo vizuri ndiyo uruhusiwe".

EATV&EA Radio Digital, ilimtafuta Mkuu huyo wa Wilaya kwa ajili ya kupanda undani wa taarifa hizo, ambapo alidai kuwa yupo kwenye kikao na akitoka basi atatupigia simu na kutueleza ni kipi kilichojiri na hatua zipi ambazo zimekwishachukuliwa hadi sasa.