Jumapili , 21st Feb , 2021

Wajumbe wa Bunge la juu la Ufaransa (SENATE) limeipongeza Tanzania kwa kuwa kinara wa masuala ya utulivu,amani,ulinzi na usalama katika eneo la maziwa makuu hususani katika maeneo ya Mashariki ya Kongo pamoja na eneo la kaskazini mwa Msumbiji.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi

Wajumbe hao ambao pia ni kundi la wabunge marafiki wa Tanzania wametoa pongezi hizo wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi alipotembelea bunge hilo na kuongeza kuwa kupitia Jumuiya za kikanda ikiwemo SADC Tanzania imekuwa kiongozi katika kuhakikisha amani kaskazini mwa Msumbuji na kwamba wajumbe hao wako tayari kuunga mkono jitihada hizo

Katika jitihada za maendeleo zinazofanywa na Tanzania wajumbe hao wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kujenga uchumi imara nakusema kuwa wako tayari kuhamasisha watalii wengi kutoka Ufaransa na Ulaya kwenda Tanzania ili kuifanya sekta hiyo kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania.

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amezungumza na uongozi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa ambalo limeonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania katika masuala ya maendeleo vijijini .

“Katika mazungumzo yetu ya leo tumeangalia maeneo mbalimbali ambayo wapo tayari kushirikiana na Tanzania ambayo ni maendeleo vijijini kwa maana ya umeme, barabra na maji vijijini  lakini pia wameonyesha utayari wakushirikiana na Tanzania katika kutoa mikopo na misaada katika kuimarisha na kukuza uchumi wa bluu” amesema Prof.Kabudi 

Prof Kabudi yupo Paris Nchini Ufaransa kwa ziara ya siku nne kutokana na mwaliko wa Waziri wa Ulaya na mambo ya Nje wa Ufaransa ambapo pia anaitumia fursa hiyo kukutana na makundi ya wafanyabiashara pamoja na taasisi za serikali na binafsi za ufaransa kuhamasisha masuala ya uwekezaji na biashara nchini Tanzania.