Ijumaa , 18th Sep , 2020

Wakazi wa Ulongoni A na B Jijini Dar es Salaam, wamewahimiza wakandarasi kuongeza juhudi ili ujenzi daraja linalounganisha maeneo hayo ukamilike ndani ya Muda uliopangwa ili kupunguza kero walizokuwa wakizipata katika nyakati za Mvua.

Muonekano wa daraja la Ulongoni.

Akizungumzia kero ya daraja hilo Mwenyekiti wa Mtaa wa Ulongoni A, Abdulahim Munis amesema kuwa daraja hilo limekuwa kero katika kipindi cha mvua hadi kupelekea watu kupoteza maisha na wengine hupoteza makazi kutokana na mto huo kuongezeka upana kila wakati.

"Ujenzi tunaomba ukamilike kwa wakati, maana adha tunayopata wakati wa mvua imekuwa ya muda mrefu ambayo hupelekea kupoteza mawasiliano kati ya wakati wa upande mmoja na mwingine na wengi wetu hukimbia makazi yao kutokana na maji kupasua kingo za mto", amesema Munis

Kwa upande wao Wakala wa Barabara Vijijini na Mijiji(TARURA) kupitia kwa mratibu wake wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo umekuwa ukisua sua kutokana na mto huo kuongezeka kila wakati hivyo katika kipindi hiki wamepata mwarobaini wa mto huo ambapo daraja litakamilika kwa wakati na kwa kiwango stahiki.

Ujenzi wa Daraja la Ulongoni A lililopo Kata ya Gongolamboto, ujenzi wake unagharimu Shilingi Bilioni 4.3 pamoja na Ujenzi wa Daraja la Ulongoni B.