Jumanne , 15th Oct , 2019

Serikali imetangaza dhamira yake ya kuwalipa wakulima 156 wa mahindi jumla ya Shilingi 315,118,510 kutokana na kudhulumiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Ndg Linus Kalandamwazye.

Wanachama wa Muzia Amcos Wilayani Kalambo.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanachama wa Muzia Amcos Wilayani Kalambo, wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Rukwa.

Malipo hayo yatawahusu wakulima wa Tarafa ya Mwimbi yenye kata nne ambazo ni Mambwe Kenya, Ulumi, Mkombo na Mwazye, kutokana na kupima mahindi yao zaidi ya Tani 622.679 kwenye Chama cha Muzia Amcos kilichopewa uwakala na serikali wa kununua mazao kwa wakulima tarehe 8 Agosti 2017 kwa makubaliano ya kulipwa ndani ya wiki tatu kutoka tarehe ya kupimwa lakini hawakulipwa mpaka sasa.

Waziri wa Kilimo Mh. Japhet Hasunga 

“Kesi ikiwa mahakamani serikali haiwezi kuingilia badala yake wakati tunaendelea na kesi hiyo ninaziagiza taasisi zangu tatu kuchanga fedha kwa ajili ya kuwalipa wakulima hao”, Alisema Mhe Hasunga.

Alisema wanaotakiwa kuchanga fedha hizo kwanza ni Wizara ya Kilimo kwa kushindwa kulishughulikia jambo hilo kwa wakati ili wakulima hao waweze kulipwa fedha zao.