Jumatatu , 18th Mar , 2019

Serikali imewahakikishia wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuwa kufikia tarehe 31 Machi 2019 wakulima wote watakuwa wamelipwa fedha zao kwani uhakiki umekamilika kwa kiasi kikubwa.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akiwa mkoani Lindi wakati akitoa ufafanuzi katika mkutano uliowakutanisha wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Dkt Christine Ishengoma.

"Kumekuwa na urasimu mkubwa tangu kuanza kwa zoezi hili la uhakiki lakini sasa tumeamua kama serikali kabla ya mwisho wa mwezi huu wa tatu wakulima wote wawe wamelipwa malipo yao ili kuondoa adha wanazokumbana nazo", amesema Waziri Hasunga.

Alisema pamoja na kwamba malipo ni mchakato unaohitaji kupitia katika hatua nyingi ikiwemo uhakiki lakini kila jambo lenye mwanzo ni lazima liwe na ukomo.

Alisema mpaka sasa, jumla ya Tani 222,684 zimekwisha kusanywa huku hadi kufikia tarehe 14 Machi 2019 tayari jumla ya Shilingi Bilioni 596.9 zimekwishalipwa kwa wakulima kati ya Shilingi Bilioni 723.