Ijumaa , 16th Aug , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo amevitaka vyama vya ushirika katika Mkoa wa Rukwa kujiunga na Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa, ili kuwa na umoja na nguvu katika kutafuta masoko ya mazao yao na kuachana na walanguzi.

Ameyasema hayo katika mkutano wa Vyama vya Ushirika mkoani humo, aliouitisha ili kuwatafutia wanachama wapya chama kikuu cha Ushirika cha Mkoa pamoja na kusikia mipango yao waliyojiwekea kuanzia mpango wa mwaka mmoja hadi miaka kumi.

Amesema kuwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa 'Ufipa Cooperative Union Ltd (UCU)' ni chama kipya na kinahitaji nguvu ya vyama vya ushirika vya mkoa mzima ili kiwe na uongozi uliokamilika.

"Mkulima ana mahangaiko makubwa sana, sasa huu ushirika ni chombo cha kumkomboa mkulima, ni chombo cha kunyanyua uchumi wa mkulima, ni chombo cha kuikomboa Rukwa, ni chombo cha kuikomboa nchi yetu ya Tanzania, nchi ambayo sasa inaelekea kwenye uchumi wa kati wa viwanda", amesema Wangabo.