Jumatano , 20th Feb , 2019

Kufuatia kushuka kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Mkoani Njombe kutoka asilimia 14 hadi asilimia 11.4 wananchi mkoani humo wamedai kuwa huenda kiwango hicho kikapanda tena kwa kile walichokidai kuwepo kwa upungufu wa upatikanaji wa Kondom.

Hali hiyo inajiri siku chache baada ya Baraza la Madiwani katika halmashauri ya Mji Makambako kuwasilisha hoja ya upungufu wa kondom ambapo walimtaka Mkurugenzi kupitia Wizara ya Afya kuwasaidia wananchi kupata huduma hiyo.

Wakizungumza na www.eatv.tv baadhi ya wananchi mkoani Njombe wamesema kutokana na jitihada za serikali juu ya kupambana na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi kuna haja serikali kuangalia namna ya kuongeza kinga muhimu.

Nao baadhi ya wahudumu wa nyumba za kulala wageni na wafanyabiashara wa Kondomu wamesema ni miezi mitatu sasa tangu kuanza kuadimika kwa bidhaa hiyo jambo ambalo limepelekea wateja kuzifuata mbali na nyumba hizo za kulala wageni tena kwa bei kubwa.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Makambako Ernest Kyungu ametolea ufafanuzi juu ya changamoto hiyo na kubainisha kuwa serikali mkoani humo inaendelea kulifuatilia.