Ijumaa , 15th Mar , 2019

Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini kupitia Msemaji wake, Ahmed Msangi wamesema watawachukulia hatua askari wake ambao wanatajwa kumbambikia kesi kijana Mussa Sadiki aliyemuandikia barua Rais Magufuli ili kumuomba msaada.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Ahmed Msangi

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam Ahmed Msangi amesema kuwa watahakikisha wahusika wa tukio hilo wanachukuliwa hatua za kisheria.

Aidha Msangi amesema,"malalamiko ya mwananchi Mussa Sadick tuliyapata kupitia DCI tukamwagiza afisa wa juu kwenda kufuatilia na afisa bado anaendelea kulishughulikia japo amekiri ni kweli yule mtu alibambikiwa kesi kwa hiyo tunafanya taratibu za kumtafuta askari aliyefanya suala lile."

"Naomba wananchi wasiogope wanapoona wanaonewa na polisi wawe wepesi kutoa taarifa inawezekana afisa mmoja ameenda kinyume na maadili ya jeshi watu wasisite kutoa taarifa." amesema Ahmed Msangi

Mapema jana baadhi ya vyombo vya habari nchini vililiripoti malalamiko ya kijana Mussa Sadick mkazi wa Tabora akilituhumu jeshi la polisi mkoani humo kumbambikia kesi.