Alhamisi , 17th Jun , 2021

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martin Shigella, amepiga marufuku mgambo wa Manispaa hiyo kuhusika na operesheni yoyote ndani ya mkoa huo hususani za ukusanyaji wa mapato badala yake wabaki kuwa walinzi wa majengo na mali za Halmashauri.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martin Shigella

Katazo hilo limekuja zikiwa zimepita siku kadhaa tu tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliposhangazwa na mgambo kwa kitendo chao cha kuharibu, kuvunja na kuwapiga wafanyabiashara waliogoma kufanya biashara katika eneo walilopangiwa hali iliyopelekea Mkuu wa wilaya ya Morogoro Bakari Msulwa na Mkurugenzi wake kufukuzwa kazi mara moja.

"Kuanzia muda huu sitaki tena kuwaona migambo wakifanya operesheni zozote ndani ya mkoa huu, Meya na Mkurugenzi kama bado mnawahitaji endeleeni kuwatumia kwenye ulinzi wa majengo na mali za Halmashauri lakini suala la makusanyo ya mapato, watu wamejipanga vibaya, wame-park katikati ya barabara ziko mamlaka zilizopewa kazi hizo, mgambo siyo kazi yao kuwatoa wananchi kwenye maeneo wanayofanya shughuli zao," amesema RC Shigella.