Alhamisi , 17th Oct , 2019

Jumla ya wanafunzi 1,890 waliosoma katika shule binafsi kwa ufadhili na wakathibitisha taarifa zao, Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESBL), kama ilivyokuwa imeagizwa na Waziri wa Elimu, Joyce Ndalichako wamekwishapatiwa mikopo.

Taarifa hiyo imetolewa leo Oktoba 17, 2019, na Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo Abdul-Razaq Badru, ambapo amesema kuwa mpaka sasa wamekwishatoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 113.5 kwa wanafunzi 30,675 wa awamu ya kwanza ya masomo kwa mwaka 2019/2020.

Katika makundi maalum pia tuna wanafunzi 1,890, sawa na asilimia 6 ya wanafunzi 30,675 wa awamu ya kwanza, ambao walisoma shule binafsi lakini kutokana na hali duni ya uchumi, walifadhiliwa na walithibitisha kwa kuweka nyaraka sahihi'' amesema Badru.

Aidha Badru amewataka waombaji wa mikopo, kufungua akaunti zao binafsi ili waweze kupata taarifa za mikopo kwa urahisi zaidi.

Pamoja na tovuti, wanafunzi wanaweza kufungua akaunti zao walizooombea mkopo mtandaoni maarufu kama SIPA na kuona walivyopangiwa na tunaanza kupeleka fedha vyuoni kesho kwa kuwa Serikali imeshatukabidhi Shilingi bilioni 125, ambazo tuliomba kwa malipo ya kati ya Oktoba hadi Disemba mwaka huu'' amesema Badru.

Kwa mwaka huu wa masomo, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 450, zinazolenga kuwanufaisha jumla ya wanafunzi 128,285, kati yao zaidi ya wanafunzi 45,000 ni wa mwaka wa kwanza na wengine 83,285 ni wanaoendelea na masomo