"Wameambukizwa Ukimwi, nitawasemea" - Matiko

Ijumaa , 15th Mar , 2019

Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko amelituhumu jeshi la polisi kwa kuwafanyia unyanyasaji wa kingono, mabinti na wanawake wanaopelekwa katika vituo vya polisi pindi wanapokamatwa.

Mbunge Esther Matiko

Akizungumza na wanahabari, leo Machi 15, Matiko amesema kwamba, alipokuwa Segerea amekutana na malalamiko ya wanawake ya kwamba wamebakwa na kulawitiwa walipokamatwa na hata kuambukizwa maradhi.

Amesema kwamba vitendo vya unyanyasaji kwa mkoa wa Dar es salaam vimekithiri katika vituo vya Sitaki Shari, Kawe na kile cha Mabatini.

Ameongeza kwamba, "licha ya kulisema suala hili leo mbele ya wanahabari, kama muwakilishi wa wanananchi Bungeni atalifikisha jambo hilo ndani ya bunge ili waathiriwa wa vitendo hivyo wapatiwe haki yao

"Kuna kesi  nyingi sana, mabinti wanabakwa kwenye vituo vya polisi, kulawitiwa na hata kuambukizwa virusi vya ukimwi, nimesema nitalisema hili  bungeni na popote pale mpaka haki za mabinti hawa zitakapopatikana" Amesema Matiko.

Pamoja na hayo Matiko amelalamikia suala la watu wenye magonjwa wa akili kuchanganywa na wemye utimamu katika magereza hasa Segerea na kusema kunaweza kupelekea matatizo kwa mahabusu au wafungwa wengine ndani ya gereza.

Ameongeza kwamba Licha ya matatizo yanayoweza kusababishwa na wagonjwa hao, Serikali inapaswa kutumia sheria ya 'Insanity ACT 31' ambayo inatamka wazi kwamba mtu anayekamatwa akawa na matatizo ya akili apelekwe sehemu stahiki na siyo magereza.

Aidha Matiko amesikitika kuwepo na mahabusu wengi magerezani huku serikali ikitumia gharama kubwa kwa mahabusu ambao hawazalishi huku akisisitiza kwamba wanawake waliopo katika magereza hayo wengine ni wazazi ambao kwa kuwekwa muda mrefu bila kujua hatima ya kesi zao kunapelekea watoto wa mitaani.