Jumanne , 26th Mei , 2020

Wamiliki wa viwanda vya kuchakata minofu ya samaki kanda ya ziwa wameiomba Serikali kuongeza ndege za mizigo ili kuwawezesha kusafirisha minofu mingi itakayosaidia kuongeza kipato chao na nchi kwa ujumla.

Ubebaji wa minofu ya samaki katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza

Wameyasema hayo wakati wakisafirisha tani 22 za minofu ya samaki iliyokuwa inaelekea nchini Ubelgiji kwa ndege namba A 330-300 ya nchini Rwanda, ndipo wakatumia fursa hiyo kuiomba serikali kuongeza ndege za mizigo ili kuhakikisha minofu hiyo inawafikia wateja wao kwa wakati.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema kuboreshwa kwa uwanja huo wa ndege wa Mwanza kunazidi kuongeza fursa za uwekezaji hivyo kuwataka wawekezaji kuitumia vizuri fursa hiyo.

"Samaki hawa sifa yake kubwa ni kufika kule wakiwa freshi, na upelekaji kwa ndege unatusaidia kuongeza sifa hiyo na kuongeza thamani ya samaki wanaotoka Tanzania", amesema John Mongella.